Yanga imegoma kabisa kufungwa ligi kuu ya Vodacom baada ya leo kuchomoa bao katika dakika ya 76 na kufanikiwa kupata alama moja muhimu ugenini katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons
Saido Ntibazonkiza 'Antibiotic' ameendelea kuonyesha thamani yake akifunga bao hilo muhimu sana

Ulikuwa mchezo mgumu uliotawaliwa na matumizi ya nguvu na ukachagizwa na changamoto ya uwanja wa Nelson Mandela
Mvua iliyonyesha muda mfupi kabla ya mchezo huo ilisababisha 'majanga' kwani unaweza kudhani wachezaji wako shambani wanavuna mpunga kumbe sivyo
Jumanne Elfadhili ndiye aliyewatanguliza Tanzania Prisons kwenye dakika ya 52, akimalizia mpira wa adhabu uliowapita walinzi wa Yanga
Kuingia kwa bao hilo kuliiamsha Yanga iliyoanza kulisakama lango Prisons wakisaka bao la kusawazisha
Hakuna ufundi uliohitajika leo kutokana na mazingira ya uwanja, mipira mirefu na krosi kupitia kwa wachezaji wa pembeni Tuisila Kisinda, Kibwana Shomari na Yassin Mustafa
Hii ni alama muhimu sana kwa Yanga ukizingatia ugumu wa mchezo huo. Nyota wa Yanga wanastahili pongezi kwa kuonyesha upambanaji na kutokata tamaa
Yanga sasa inaonyesha tabia ya 'kibingwa', hakua kukata tamaa mpaka mwisho..!