Vinara wa ligi kuu ya Vodacom Yanga wana jambo lao mkoani Rukwa jioni ya leo watakaposhuka uwanja wa Nelson Mandela kuikabili Tanzania Prisons
Huu ni mchezo wa mwisho kwa mwaka 2020, pia ukiwa mchezo wa pili baina ya timu hizo msimu huu
Timu hizi zilikutana katika mchezo wa kwanza kabisa wa ufunguzi wa msimu na mchezo kumalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1 pale uwanja wa Benjamin Mkapa
Hata hivyo yapo mabadiliko makubwa yamefanyika katika kikosi cha Yanga kilichocheza na Prisons wakati ule
Wananchi sasa wako chini ya mtaalam Cedric Kaze ambaye kwa kiasi kikubwa ametengeneza timu imara inayoshikilia usukani wa ligi tangu mwezi uliopita
Wakiwa timu pekee ambayo haijapoteza mchezo, Wananchi wamepania kuendeleza mwenendo huo wakifahamu wanaanza duru ya lala salama
Yanga leo inaweza kuwasoka wachezaji wake watatu Saido Ntibazonkiza, Yacouba Sogne na Ditram Nchimbi ambao taarifa ilitolewa juzi kuhusu changamoto zinazowakabili
Saido na Yacouba waliumia katika mchezo dhidi ya Ihefu Fc, wakati Nchimbi alipata matatizo ya kifamilia huku mlinda lango Ramadhani Kabwili nae akiwa majeruhi
Saido na Yacouba waliatarajiwa kuangaliwa zaidi baada ya mazoezi ya mwisho kuona kama wanaweza kutumika leo
Ukiondoa wachezaji hao, kikosi cha Kaze kiko imara kuelekea mchezo huo ambao utaunguruma kuanzia saa kumi Alasiri
Prisons imekuwa na matokeo mazuri katika mechi walizocheza katika uwanja wa Nelson Mandela, wamefungwa mara moja tu
Ni timu inayofahamika kwa kucheza soka la nguvu, unaweza kuwafananisha na Dodoma Jiji ambao walichezea kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Yanga mkoani Arusha
Hivyo hautakuwa mchezo mwepesi, lakini ni mchezo ambao Yanga inahitaji matokeo ya ushindi ili kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi