Vinara wa ligi kuu ya Vodacom Yanga wako mkoani Mbeya ambapo leo watashuka kunako uwanja wa Sokoine kuikabili Ihefu Fc katika mchezo wa kukamilisha duru ya kwanza
Mchezo huo utapigwa mapema, kuanzia saa tisa Alasiri
Hii ni nafasi nyingine kwa Yanga kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo mpaka sasa wakiwa juu kwa tofauti ya alama nane dhidi ya watani zao Simba ambao wao watakuwa kule Zimbabwe kuumana na Platinum Fc katika mchezo wa ligi ya mabingwa
Yanga ilitua mkoani Mbeya juzi, siku ya jana wachezaji wakapata nafasi ya kufanya mazoezi ya mwisho katika uwanja wa Sokoine
Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo ambao wanatarajia hautakuwa mwepesi
Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo msimu huu. Ukiwa ni mchezo wa kukamilisha duru ya kwanza, Wananchi hawatakuwa tayari kuchafua rekodi yao hiyo ya kipekee