Kiungo mshambuliaji wa Yanga Saido Ntibazonkiza kesho anatarajiwa kuendeleza makali yake katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ihefu Fc ambao utapigwa uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya
Ntibazonkiza aliwasili Mbeya jana akiwa sambamba na kikosi cha wachezaji wengine wa Yanga
Pamoja na kucheza barani Ulaya kwa muda mrefu, Ntibazonkiza ameanza maisha yake Yanga kwa kucheza katika viwanja vyenye changamoto
Lakini hilo halikumzuia kuonyesha ubora wake kwani katika michezo miwili, amefunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao
Mchezo dhidi ya Ihefu utakuwa wa tatu hapa nchini na hakuna shaka Cedric Kaze atampa nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza
Mwamba huyu yuko katika kiwango bora kwani amefunga katika mechi tano mfululizo
Alianza kuwatungua Stars kwenye mchezo kirafiki jijini Dar es salaam, alijiunga na Yanga baada ya mchezo huo
Kisha akarejea Burundi kwa ajili ya majukumu ya timu ya Taifa katika michuano ya kuwania tiketi ya Afcon 2021
Akaweka kambani kwenye mchezo wa ugenini dhidi ya Mauritania, mchezo ambao Burundi ilifanikiwa kupata sare ya bao 1-1
Timu hizo ziliporudiana kule Burundi Ntibazonkiza akaweka kambani mabao mawili na kuisaidia Burundi kuondoka na ushindi wa mabao 3-1
Baada ya kumaliza majukumu ya timu ya Taifa ndipo akatua nchini kujiunga rasmi na Wananchi ambapo mchezo wake wa kwanza ulikuwa dhidi ya Singida United ukiwa mchezo wa kirafiki
Katika mchezo huo uliopigwa mkoani Singida, Ntibazonkiza akaweka kambani mabao mawili
Shoo akaiendeleza kule Arusha dhidi ya Dodoma Jiji akifunga bao moja na kutengeneza jingine katika mchezo wake wa kwanza ligi kuu ya Tanzania Bara
Amefunga mabao saba katika mechi hizo tano ambazo kila moja aliweka kambani