Usajili wa Saido Ntibazonkiza umelipa mapema tu, kwani katika mchezo wake wa kwanza kwenye ligi, amefunga bao moja na pia katoa pasi ya bao la Bakari Nondo Mwamnyeto
Huo ulikuwa mchezo wa pili kwa Ntibazonkiza kuitumikia Yanga, wa kwanza ulikuwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Singida United ambapo alifunga mabao mawili na hivyo ndani ya mechi mbili amehusika katika mabao manne!
Hizi ni takwimu za kutisha! Unaweza kusema huko mbeleni kuna timu zitashushiwa ghalika kwani Yanga hii ya kina Ntibazonkiza inatisha!
Sasa jana baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji, Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said akatamba kuwa usajili wa Ntibazonkiza waliufanya kimkakati, na kuwa wananchi wafurahie matunda yake
Lakini pia Injinia Hersi amesema katika kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo, wamekusudia kumshusha nyota mwingine ambaye yuko katika kiwango cha Ntibazonkiza
Yanga inapiga hesabu za aina mbili, moja ni kutengeneza kikosi ambacho kitatwaa ubingwa, pili ni kutengeneza kikosi ambacho kitatikisa michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao
Wananchi wanataka kuwa klabu ya kwanza hapa nchini kushinda taji hilo kubwa zaidi barani Afrika kwa ngazi ya vilabu
Pamoja na kuwa kocha Cedric Kaze anaendelea kukijenga kikosi chake, Yanga imeanza kuonyesha sura ya kibingwa