GSM, uongozi wa Yanga, Wanachama pamoja na mashabiki wana kila sababu ya kufurahia matunda ya uvumilivu wao walioonyesha wakati wakimsubiri kocha Cedric Kaze
Kaze raia wa Burundi,alisubiriwa na Wanayanga kwa vipindi viwili tofauti
Awali alitangazwa kuwa ndiye mrithi wa Luc Eymael ambaye alitimuliwa mwishoni mwa msimu uliopita baada ya kutoa matamshi ya kibaguzi dhidi ya Mashabiki wa Yanga
Kaze alisubiriwa kwa takribani wiki tatu lakini dili lake la kutua Yanga likavurugika dakika za mwishoni baada ya kupata changamoto ya kuuguliwa na mkewe
Kaze aliomba asubiriwe kwa wiki nyingine tatu, jambo ambalo lilikuwa gumu kutekelezeka kwa Wadhamini GSM na uongozi wa Yanga kwani msimu mpya ulikuwa mbioni kuanza
Hiyo ikawa sababu kwa GSM kusaka kocha 'fasta-fasta', wakimleta nchini Zlatko Krmpotic ambaye hata hivyo mbinu zake hazikukubalika na kuonyeshwa mlango wa kutokea baada ya siku 37 tu tangu apewe majukumu ya kuinoa Yanga
Hii ikawa nafasi nyingine kwa Yanga kumrudia Kaze, hata hivyo; kukawa na wiki nyingine tatu za kumsubiri
Hatimaye Oktoba 16, Kaze akatua nchini na tangu wakati huo amewaongoza wananchi katika michezo 10 ya ligi bila kufungwa
Katika michezo hiyo ameshinda saba, amepata sare tatu na hakufungwa mchezo wowote
Ameikusanyia Yanga alama 24 kati ya alama 30, sasa kikosi chake kikiwa kileleni mwa msimamo wa ligi na alama 37
Ukiitizama Yanga inavyocheza, sasa utakubali ilikuwa sahihi kumsubiri mtaalamu huyu wa tiki-taka kutoka kule Fc Barcelona
Kaze amekiimarisha kikosi cha Yanga, 'mziki' wa Wananchi umeanza kuwatia hofu wapinzani wao katika mbio za kuwania ubingwa
Kwa jinsi Yanga inavyocheza, ni timu ambayo inaweza ikaandika rekodi msimu huu kwani hawaonekani kama timu inayoweza kufungwa leo wala kesho