Jioni ya leo Jumamosi, Disemba 12, Wananchi wana jambo lao mkoani Shinyanga wakitarajiwa kushuka katika uwanja wa CCM Kambarage kuikabili Mwadui Fc katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Yanga ilitua Shinyanga juzi usiku, jana ikapata nafasi ya kufanya mazoezi ya mwisho hapo CCM Kambarage
Mkufunzi wa Yanga Cedric Kaze amesema vijana wake wana ari ya kusaka alama tatu kwenye mchezo huo ambao wanatarajia kupata upinzani mkali kutoka kwa wenyeji wao
Mwadui Fc ina mwenendo wa kusuasua msimu huu, ni timu iliyofungwa mabao mengi zaidi, wakiruhusu mabao 28 huku wenyewe wakifunga mabao 11
Wanashika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 10. Wanakutana na Yanga inayoongoza ligi ikiwa imekusanya alama 34 pia ikiendelea kushikilia rekodi ya kutofungwa msimu huu
Lakini mchezo hautarajiwi kuwa mwepesi kwa Yanga, kwani ni kawaida kila timu inayokwenda kupambana na Yanga, huchukulia mechi hiyo kama fainali
Kocha wa Mwadui Fc ametamba kuwa timu yake leo inakwenda kuichafulia Yanga rekodi yake ya kutofungwa
Kaze yuko Shinyanga na kikosi chake kamili ambacho kimempa matokeo katika michezo mitatu iliyopita. Wananchi wamedhamiria kuodoka na alama zote tatu