Ifikapo Jumatano ya wiki ijayo, dirisha dogo la usajili litakuwa wazi ambapo timu za ligi kuu zitakuwa na nafasi ya kuimarisha vikosi vyao kuelekea ngwe ya lala salama kukamilisha msimu
Ni wakati ambao Wanayanga wanausubiri kwa hamu kufahamu kocha Cedric Kaze atamuongeza nani katika kikosi chake ili kuwahakikishia Wananchi ubingwa mwishoni mwa msimu
Tayari Kaze amemsajili Saido Ntibazonkiza, usajili huo ukifanyika mapema tu baada ya kocha huyo wa zamani wa Academy ya Fc Barcelona kutua Yanga
Lakini imeelezwa Yanga inaweza kuongeza nyota wengine watatu ili kuboresha maeneo yenye changamoto
Aidha baadhi ya wachezaji wanaweza wakatolewa kwa mkopo katika vilabu vingine ambako watapata nafasi ya kucheza ili kuimarisha viwango vyao
Orodha ya wachezaji hao inawahusu nyota kama Adeyum Saleh, Abdulaziz Makame 'Bui', Juma Mahadhi na Waziri Junior wote wakikosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza
Mlinda lango Farouk Shikhalo nae ameshindwa kutamba mbele ya Metacha Mnata pengine haitashangaza kama dirisha dogo ataruhusiwa kwenda kutafuta changamoto kwingine
Shikhalo amecheza mechi moja tu ya ligi msimu huu, mchezo wa ufunguzi ambao Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons
Yanga ina nafasi moja ya mchezaji wa kigeni iliyo wazi, hivyo wanaweza kuchukua uamuzi wa kumruhusu Shikhalo ili wasajili mchezaji mwingine wa kigeni asiye golikipa
Maeneo ambayo yanatajwa kuwa yataongezwa nguvu ni pamoja na safu ya ulinzi upande wa kushoto, Mnyarwanda Eric Rutanga ambaye usajili wake ulikwama mwezi August, anatajwa kurejea katika mipango ya Wananchi
Pia nafasi ya kiungo mchezeshaji na mshambuliaji wa kati. Eneo la ushambuliaji ndio nafasi ambayo ni kilio cha Wanyanga wengi kutokana na uhaba wa mabao kwa washambuliaji waliopo licha ya kuwa yapo maboresho yameanza kuonekana katika eneo hilo
Kaze amewapa changamoto washambuliaji wake wamshawishi asisajili mshambuliaji mwingine kwa kuhakikisha wanafunga mabao mengi zaidi
Moto wao ulionekana kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Jumamosi watakuwa na nafasi nyingine kwenye mchezo dhidi ya Mwadui FC