Wananchi leo wana jambo lao pale uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Ruvu Shooting ambao utapigwa kuanzia saa moja usiku
Vinara hao wa ligi kuu watakuwa na nafasi ya kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi katika muda huu wa lala salama kuelekea kukamilisha duru ya kwanza
Ni mechi nne zimebaki kukamilisha duru ya kwanza. Wananchi wakimaliza mechi ya leo mechi nyingine zinazofuata ni dhidi ya Mwadui Fc, Dodoma Jiji na Ihefu Fc
Mabingwa hao wa kihistoria watafunga mwaka kwa kucheza mchezo mmoja wa duru ya pili dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa Disemba 31
Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amewaandaa vijana wake kwa wiki nzima baada ya mchezo dhidi ya JKT Tanzania walioshinda kwa bao 1-0
Kaze anaingia kwenye mchezo huo akiwa na kikosi chake kamili, mpango uliopo ni kuhakikisha alama zote tatu zinabaki nyumbani
Hata hivyo hautakuwa mchezo mwepesi hasa ikizingatiwa kuwa Ruvu Shooting inanolewa na kocha Charles Mkwasa ambaye anaifahamu vizuri Yanga
Aliondoka Yanga mwanzoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake kumalizika
Mkwasa ni muumini wa soka la kushambulia na hivyo ndivyo Ruvu Shooting inavyocheza. Haishangazi kuona timu hiyo inashika nafasi ya nne ikiwa na alama 23 sawa na Simba
Mashabiki wa Yanga wameaswa kujitokeza kwa wingi uwanja wa Mkapa ili kuwapa sapoti wachezaji wao kuhakikisha wanaibuka na ushindi
Mchezo utapigwa kuanzia saa moja usiku