Ukweli ni kwamba tangu kuwasili kwa kocha Cedric Kaze, yapo mabadiliko makubwa ambayo kikosi cha Yanga kimeyaonyesha
Utaona kwa sasa Yanga inatengeneza nafasi nyingi sana ukilinganisha na awali ilipokuwa ikinolewa na Zlatko Krmpotic
Kipindi kile Yanga ilitegemea zaidi mipira ya adhabu na kona kufunga mabao
Changamoto iliyopo sasa ni matumizi ya nafasi hizo. Mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania Yanga ingeweza kufunga sio chini ya mabao manne kama washambuliaji wake wangekuwa makini
Kocha Kaze ameonyesha kukerwa na ubutu wa washambuliaji akiahidi kuendelea kusahihisha mapungufu yanayojitokeza lakini pia akiwataka nao waongeze umakini langoni
Mechi za karibuni Yanga imebebwa na viungo Carlinhos na Deus Kaseke ambao ndio waliofunga mabao katika mechi tatu zilizopita
Pamoja na ujio wa Saido Ntibazonkiza, ni wazi Kaze anaweza kusajili mshambuliaji mwngine dirisha dogo ili kuongeza nguvu
Jina la Heritier Makambo limerejea kwenye 'headlines' kwa mara nyingi ikielezwa hata baadhi ya wachezaji waandamizi wamependekeza nyota huyo arejeshwe kikosini
Makambo ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao ya vichwa, Yanga ya sasa inazalisha mipira mingi ya krosi lakini matumizi yamekuwa madogo