Mchezaji nyota wa zamani wa kandanda Diego Maradona amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 60.
Kiungo huyo mshambuliaji wa Argentina awali mwezi huu alifanyiwa upasuaji wa ubongo ambao madaktari walimwambia ulifaulu
Baada ya upasuaji huo, ilitangazwa kuwa Maradona angeanza matibabu ya uraibu wa pombe
Maradona ni moja ya wachezaji bora zaidi wa kandanda kuwahi kutokea
Mwaka 1986 akiwa nahodha wa Argentina, aliliongoza Taifa lake kushinda Kombe la Dunia nchini Mexico huku akionesha uwezo binafsi mkubwa katika ushindi huo.
Alizichezea klabu za Barcelona ya Uhispania na Napoli ya Italia. Akiwa na Napoli alinyakua ubingwa wa ligi ya Serie A kwa misimu miwili. Maradona aliifungia Argentina magoli 34 katika michezo 91, akishiriki michuano minne ya Kombe la Dunia

Aliliongoza Taifa lake katika fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 1990 nchini Italia, ambapo walifungwa na Ujerumani Magharibi.
Alikuwa tena nahodha wa taifa lake katika mashindano ya 1994 nchini Marekani lakini alirudishwa nyumbani baada ya kubainika alitumia dawa za kuongeza nguvu.
Katika miaka yake ya mwisho ya uchezaji aligubikwa na utumiaji wa dawa za kusisimua misuli pamoja na dawa za kulevya.
alitaabika na matumizi na uraibu wa dawa za kulevya aina ya cocaine na alifungiwa kucheza mpira kwa miezi 15 baada ya kubainika kuwa alikuwa akitumia dawa hizo mwaka 1991.
Alistaafu kusakata kandanda la kulipwa mwaka 1997 katika siku ya kuadhimisha miaka 37 ya kuzaliwa kwake, akiwa na klabu maarufu nchini Argentina ya Boca Juniors
Buriani Maradona..!