Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema walistahili kupata ushindi kwenye mchezo dhidi ya Namungo Fc lakini makosa waliyofanya yaliinufaisha Namungo kupata alama moja
Akiingoza Yanga katika mchezo wa sita, Kaze alijikuta akidondosha alama nyingine mbili na hivyo kumfanya awe ameacha alama sita katika michezo mitatu iliyopita
Amesema sare dhidi ya Namungo sio matokeo waliyotarajia kwani walihitaji kupata ushindi ili kuweza kuongoza ligi
Hata hivyo anaamini bado timu yake ina nafasi ya kufanya vizuri kwani kuna mechi nyingi mbele
"Tulitamani kupata alama tatu ili kukaa juu ya msimamo wa ligi lakini haikuwezekana. Baada ya kupata bao tulishindwa kujipanga na kuwapa nafasi Namungo ya kusawazisha"
Kuna makosa kadhaa tumeyafanya, ligi ni Marathon tunajipanga kwa ajili ya mchezo ujao"
"Bado mechi sita kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa muda ukifika tutajua tumuongeze nani ila kwa sasa tupo na wachezaji wetu hawa hawa," alisema Kaze
Keshokutwa Jumatano, Yanga itakuwa na mchezo mwingine wa ligi dhidi ya vinara wa ligi hiyo Azam Fc, mchezo ambao Wananchi hawatahitaji tena sare