Uongozi wa klabu ya Yanga SC, umemtangaza Hajji Mfikirwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu mpya ambaye anachukua nafasi ya Wakili Simon Patrick ambaye amesimamishwa kazi.
Wakili Simon amesimamishwa kazi siku tatu zilizopita akituhumiwa kuhujumu timu hali iliyopelekea kuundwa Kamati huru kwa ajili ya kuchukunguza suala hilo kabla ya kutolewa hukumu
Akizungumza na Wanahabari mapema leo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela amesema Kamati ya Utendaji inamuamini Hajji ataweza kuipeleka mbele klabu hiyo kutokana na uwezo mkubwa alionao.
Mwakalebela ameliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuzifanyia kazi kesi zao walizoziwasilisha ambazo ni ile ya Ramadhani Kabwili, pamoja na mkataba wa Bernard Morrison kwa kuwa wanaelekea katika dirisha dogo la usajili.
Mwakalebela ameongeza kuwa kama suala la Morrison ambalo limefikishwa Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo ya FIFA (CAS) kama lisipofanyiwa kazi mpaka dirisha la usajili likafunguliwa huenda mkataba ukabadilishwa kwa kuwa muda utapatikana dirisha likiwa wazi
Ripoti ya Mapendekezo ya Mabadiliko iko tayari
Katika hatua nyingine, Mshauri wa Yanga Senzo Mazingisa amesema anatarajiwa kusafiri kwenda nchini Hispania wiki ijayo kuchukua ripoti ya Mapendekezo ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kutoka wa kampuni ya La Liga
Mazingisa amesema baada ya kuipata ripoti hiyo, hatua itakayofuata ni kuiweka wazi kwa wadau waweze kutoa maoni yao kabla ya kuipeleka mbele ya wanachama wa Yanga kwa ajili ya maamuzi
Mazingisa pia alizungumzia mchakato wa Ujenzi wa kampasi ya Yanga Kigamboni ambapo amesema tayari Makampuni yameanza kujitokeza kuomba tenda iliyotangazwa na Yanga mapema wiki hii