Juzi kupitia chombo kimoja cha habari, aliyekuwa kocha wa zamani wa Yanga Mwinyi Zahera alithibitisha kulipwa madai yake yote kunako klabu hiyo
Zahera aliondoshwa Yanga mwezi Novemba mwaka jana baada ya Yanga kutolewa na Pyramids Fc michuano ya kombe la Shirikisho
Mcongomani huyo ambaye kwa sasa ameweka makazi yake Tanzania akiwa Mkurugenzi wa Ufundi klabu ya Gwambina Fc, alisema yeye na Yanga sasa hawana matatizo kwani fedha alizokuwa akidai baada ya kuvunjiwa mkataba, amelipwa zote
"Ni kweli tumemaliza na Yanga, sidai kitu, stahiki zangu zote ambazo zilikuwa kwenye maandishi ndani ya mkataba nimelipwa. Kulikuwa na pesa zingine ambazo nilikuwa natoa nje ya mkataba, kwa sababu haziko kwenye maandishi mimi siwezi kudai, ni kwamba nilitoa kwa mapenzi yangu kwa klabu ambayo naipenda," alisema Zahera
Aidha Zahera alibainisha kuwa fedha zote alizolipwa amezipeleka kwenye vituo kadhaa vya soka vya kulelea vijana 'academy', vilivyopo hapa nchini.
"Sijatumia hata senti moja, zote zimezipeleka zikasaidia soka la vijana hapa nchini, ni mchango wangu kwa ajili ya kuinua soka la Tanzania," alisema
Moja ya mambo yanayomfanya Zahera kuwa tofauti sana ni moyo wake wa kusaidia panapokuwa na changamoto
Kwa hakika Wanayanga hawatamsahau Mcongomani huyu kwani kwa kiasi kikubwa alichangia amsha-amsha ya mabadiliko Yanga
Ni yeye aliyependekeza utaratibu wa mashabiki kuichangia timu ambao ulipelekea kuandaliwa tukio la Kubwa Kuliko
Ni katika Kubwa Kuliko GSM waliingia rasmi Yanga wakitoa mchango wa Tsh Milioni 300