Jioni ya leo Yanga itashuka uwanja wa Benjamin Mkapa kuwakabili watani zao wa jadi Simba katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Huu ni mtihani wa kwanza kwa kocha Cedric Kaze ambaye alijiunga na Yanga mwezi uliopita akiachukua nafasi ya kocha aliyetimuliwa Zlatko Krmpotic
Mashabiki wa Yanga wanasubiri kukifahamu kikosi chao kinachokwenda kuanza mchezo huo
Akiwa ameiongoza Yanga kwa michezo minne Kaze tayari amepata kikosi chake cha kwanza ambacho bila shaka siku ya leo atakitumia
Langoni hakutarajiwi kuwa na mabadiliko kwani Metacha Mnata amekuwa katika kiwango bora sana
Safu ya ulinzi pia haitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa, Kibwana Shomari, Yassin Mustafa, Lamine Moro na Bakari Nondo Mwamnyeto wametumika pamoja katika mechi karibu zote ambazo Yanga imecheza mpaka sasa msimu huu
Mkongomani Mukoko Tomombe na Feisal Salum ndio pacha ya kiungo inayotarajiwa leo huku Tuisila Kisinda na Farid Mussa wakipewa nafasi kubwa ya kuanza kama viungo washambuliaji wa pembeni
Kama Kaze ataamua kuanza na mfumo wa 4-4-2 ni wazi Michael Sarpong na Yacouba Sogne wanaweza kuanza pamoja katika safu ya ushambuliaji
Lakini kama ataamua kutumia mshambuliaji mmoja, tunaweza kushuhudia Zawadi Mauya akianza sambamba na kina Mukoko na Feisal
Katika mchezo wa leo Haruna Niyonzima anakosekana akiwa mgonjwa wakati Carlinhos amerejea kikosini hivi karibuni akitoka kwenye majeraha
Kaze amethibitisha kuwa hatarajii kumtumia katika mchezo wa leo
Lakini pia wachezaji kama Deus Kaseke, Waziri Junior na Ditram Nchimbi wanaweza kuwa sapraizi kwenye kikosi cha kwanza kutegemea na mpango wa mchezo atakaokuja nao Kaze
Huu ni mchezo ambao Yanga inahitaji kushinda hivyo Kaze anapaswa kuchanga karata zake vyema ili kuhakikisha Wanayanga watakaofurika uwanja wa Mkapa wanarudi na nyuso za furaha majumbani kwao