Rekodi nyingine ya mechi za watani wa jadi inakwenda kuandikwa uwanja wa Benjamin Mkapa jioni ya leo pale Mabingwa wa kihistoria Yanga watakapowakaribisha watani zao, mabingwa watetezi Simba katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Mchezo huu utakaopigwa kuanzia saa 11 jioni, ni wa kwanza kuzikutanisha timu hizo msimu huu
Yanga iliyoanza msimu kibabe, ikiwa mwenyeji, imepania kuondoka na alama zote tatu ili kuendeleza mwenendo mzuri walioanza nao
Aidha huu ni mchezo wa kisasi kwao, wakikumbuka kipigo cha mabao 4-1 walichopokea kutoka kwa watani zao hao katika mchezo wa mwisho waliokutana msimu uliopita katika michuano ya kombe la FA
Kocha Cedric Kaze amesema wanafahamu hautakuwa mchezo rahisi kwao lakini anaamini kwa maandalizi waliyofanya, watawapa furaha mashabiki wao watakaojitokeza kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa kuwashangilia
Kaze ataingia katika mchezo huo akiwa na kikosi chake kamili japo atawakosa baadhi ya wachezaji akiwemo kiungo Muangola Carlos Carlinhos ambaye hayuko fit, Haruna Niyonzima anayeugua Malaria na Mapinduzi Balama aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu
Ushindi kwa Yanga leo, utawahakikishia kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi kuu
Ni saa 11 jioni pale uwanja wa Benjamin Mkapa