Kikosi cha Yanga kiliwasili mapema jana jijini Mwanza wakitokea jijini Dar es salaam yalipo Makao yao Makuu
Baadae leo watakuwa na jambo lao pale uwanja wa CCM Kirumba, wakishuka uwanjani kumenyana na KMC katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
KMC ndio wenyeji wa mchezo huo, wamehamishia makazi yao jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo dhidi ya Yanga
Hata hivyo ni Yanga inayoonekana kuwa nyumbani kutokana na shamrashamra za mashabiki wake
Ni mchezo unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali kutokana na ushindani uliojengeka baina ya timu hizo katika misimu miwili
Msimu uliopita KMC hawakupoteza mchezo wowote dhidi ya Yanga, walishinda mchezo mmoja wa ligi, sare moja na kushinda mechi moja ya kirafiki
Hata hivyo wanakwenda kukutana na Yanga nyingine kabisa ambayo imesukwa upya, sasa ikiwa chini ya kocha Cedric Kaze
Ni Yanga yenye malengo makubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu
Yanga ambayo imeshinda mechi tano mfululizo kwenye ligi, iko katika nafasi ya pili ikiwa imejikusanyia alama 16
Mchezo huo utashuhudiwa na Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla pamoja na viongozi wengine waandamizi wa mabingwa hao wa kihistoria
Ni saa kumi Alasiri leo mtanange utapigwa CCM Kirumba