Awamu ya pili ya kampeni ya kusaka ubingwa wa 28 ligi kuu ya Vodacom inazinduliwa rasmi leo pale uwanja wa Uhuru wakati Yanga itakapokuwa mwenyeji wa Polisi Tanzania
Awamu ya kwanza iliongozwa na kocha Zlatko Krmpotic ambaye katika mechi tano alizowaongoza Wananchi, alifanikiwa kushinda michezo minne na sare moja
Alikusanya alama 13 na kuiacha Yanga salama kwenye nafasi ya tatu. Kazi yake aliifanya vyema lakini hakufikia malengo
Ndio maana akaletwa Cedric Kaze maarufu 'Guardiola wa Kirundi', fundi wa 'pira' la tiki-taka, ametokea jikoni kabisa viunga vya Fc Barcelona ambako soka hilo ndio asili yake ilipo
Kaze anakuwa kiongozi wa awamu ya pili ya kampeni ya kuurejesha ubingwa Jangwani baada ya ubingwa huo kupotea njia kwa misimu mitatu mfululizo
Ni awamu ambayo itapeleka machungu kwa timu pinzani kwani, Kaze ameahidi hatakuwa na huruma kwa yeyote atakayekuja mbele yake
Leo majira ya saa kumi Alasiri pale uwanja wa Uhuru, Polisi Tanzania wanaweza kuwa wa kwanza kuonja 'joto ya jiwe'
Ni mchezo wa ligi kuu ya Vodacom, mzunguuko wa saba
Huu sio mchezo wa kukosa, kuna vitu havihitaji kuhadithiwa, kwani uhakika uliopo, leo rasmi mashabiki wa Yanga wataanza kuishuhudia ile timu yaooo waliyokuwa wakiisubiri
Tiketi za mechi hiyo zilianza kuuzwa tangu jana, Mzunguuko ni Tsh 5,000/-, VIP B ni Tsh 10,000/- na VIP A ni Tsh 15,000/-
Shoo iko uwanja wa Uhuru Alasiri ya leo, Mwananchi unakosaje?