Usajili wa washambuliaji Yacouba Soghne na Michael Sarpong ulipokelewa kwa shangwe na mashabiki wa Yanga, wakiamini sasa wamepata wakombozi katika safu yao ya ushambuliaji
Ni kwa sababu ya changamoto ambayo Yanga ilipitia msimu uliopita. Safu yake ya ushambuliaji ilionekana kukosa makali katika kuzifumania nyavu
Usajili huu ulipewa baraka kwa asilimia 100 na kocha wa sasa wa Yanga Cedric Kaze ambaye alishiriki katika usajili wa Yanga kwani ndiye aliyetarajiwa kuinoa Yanga kabla ya ujio wa Zlatko Krmpotic
Hata hivyo Soghne na Sarpong hawajaanza na kasi ile iliyokuwa ikitarajiwa na wengi
Sarpong amefunga mabao matatu, moja kwenye ligi na mawili katika michezo ya kirafiki

Yacouba yeye ana bao moja mpaka sasa akilifunga kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union
Kaze, mkufunzi wa Yanga amefunguka sababu ya kutong'ara kwa washambuliaji hao ni kutokana na mfumo uliokuwa ukitumiwa na kocha aliyepita
Mrundi huyo amesema anaamini wachezaji hao wana uwezo mkubwa ndio maana alipendekeza wasajiliwe, mashabiki wasubiri kuona nini watafanya chini yake
"Sarpong na Yacouba wote ni washambuliaji wazuri na wanalijua goli vizuri tu, mimi ndiye nilipendekeza wasajiliwe baada ya kuwafuatilia muda mrefu"
'Kilichotokea hadi wanaonekana wachezaji wa kawaida ni kwa sababu walikosa mbinu pamoja na viungo wa kuwawekea pasi za kufunga hali iliyosababisha hayo yote kutokea. Naamini mbinu tunazotumia sasa zitabadilisha kila kitu na mtauona ubora wao," amesema Kaze