Kocha Mkuu wa Yanga, Mrundi Cedric Kaze, tayari ameanza kukipa kikosi chake dozi ya mazoezi wakati huu mashabiki wakitazama namna atakavyoweza kuanza kukiongoza kikosi hicho kwa kulinganisha na rekodi ya kutopoteza mechi yoyote ya mtangulizi wake, Mserbia Zlatko Krmpotic
Achilia mbali rekodi ya kutopoteza pia kwenye mechi za kirafiki Krmpotic aliyoiweka Yanga tangu atue wiki moja kabla ya msimu kuanza, lakini pia Mserbia huyo hakupoteza mchezo wowote kati ya mitano ambayo aliiongoza timu hiyo, akishinda minne na kutoka sare moja.
Hivyo, Kaze ambaye alitua Yanga Alhamisi ya wiki iliyopita, tayari amenza kazi ya kukinoa kikosi hicho ambacho kinashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kikiwa na alama 13 sawa na Simba iliyopo nafasi ya pili kutokana na kuizidi kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mtangulizi wake Krmpotic, licha ya mafanikio aliyopata, soka lake lilikuwa halivutii na ni moja ya sababu iliyopelekea uongozi wa Yanga umtimue baada ya siku 37 tu
Kaze amewaahidi mashabiki kuwa watafurahia soka la burudani na ushindani, huku nae akihitaji muda kuweza kukiunganisha kikosi hicho
Kibarua chake cha kwanza kitakuwa dhidi ya Polisi Tanzania katika Uwanja wa Mkapa Alhamisi wiki hii kabla siku tatu baadaye kuifuta KMC FC kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza.
KMC imechagua kutumia Uwanja wa CCM Kirumba kama wake wa nyumbani katika mchezo huo kutokana na kanuni kuruhusu kila klabu kama ikiamua inaweza kucheza mechi mbili nje ya uwanja wake wa nyumbani inaoutumia.
Yanga itakutana na Polisi Tanzania iliyopo nafasi ya saba baada ya kucheza mechi tano na kujikusanyia alama 10, huo ukiwa ni mtihani wa kwanza kwa Kaze.
Mtangulizi wake Krmpotic mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara, yeye alipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons kisha kushinda 1-0 dhidi ya Mbeya City mechi zote zikipigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Baada ya mechi hiyo, Krmpotic akashinda 1-0 ugenini dhidi ya Kagera Sugar katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kabla ya kupata ushindi kama huo dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye dimba la Jamhuri, Morogoro na hatimaye kuivurumusha Coastal Union 3-0 Uwanja wa Mkapa.
Hivyo, kwa Kaze baada ya mechi hizo mbili dhidi ya Polisi Tanzania na KMC FC, kibarua pengine kigumu na presha kubwa kitakuwa dhidi ya ya watani zao wa jadi, Simba katika mchezo unaofuata kwenye Uwanja wa Mkapa.
Kaze amesisitiza kikubwa anachohitaji kwa sasa ni sapoti kutoka kwa mashabiki, uongozi pamoja na wachezaji ili aweze kuwapa kile ambacho wanakihitaji ndani ya uwanja.