Baada ya kutambulishwa leo, Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema miongoni mwa mambo ambayo atahitaji kuyaona katika timu yake ni wachezaji kucheza pamoja kama timu na sio mchezaji mmoja mmoja
Akizungumza mapama leo baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili, Kaze amesema falsafa aliyokuja nayo ni timu kumiliki mpira na kushambulia
Amesema katika kila mchezo atachagua timu bora na sio wachezaji 11 bora
"Nataka timu yangu imiliki mpira, icheze mpira, itengeneze nafasi. Nataka timu yangu itawale uwanja, nataka wakati tunacheza timu yangu iwe mbali na goli langu"
"Sitachezesha wachezaji 11 bora uwanjani bali nitachezesha timu bora uwanjani. Sitachezesha jina wala staa, nitachezesha timu ambayo italeta mafanikio na usishangae mchezaji mkubwa akawa anakaa benchi. Tutaangalia timu zaidi," alisema Kaze
Aidha Kaze ameweka wazi kuwa anautaka ubingwa wa ligi kuu huku akitamba kuwa na kikosi bora kilichosheheni wachezaji wazuri wanaomfanya asitamani mchezaji yeyote nje ya Yanga
"Kitu cha kwanza kwa kocha yeyote ni kutwaa ubingwa wa ligi, kwa maana ubingwa hukupa tathmini ya kikosi chako na kutambua consistency. Kwa leo nafurahia wachezaji wangu nilionao, hakuna mchezaji nnayeweza kumtamani nje ya Yanga. Nina vijana wazuri na wenye uwezo mkubwa"