Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeshindwa kujadili shauri linalomuhusu Bernard Morrison
Katika hukumu ya kesi ya mgogoro wa kimkataba kati yake na klabu ya Yanga, pamoja na kumtangaza mchezaji huyo kuwa huru baada ya kubaini mapungufu kwenye mkataba wake na Yanga, Kamati ya Sheria na hadhi za wachezaji ilimfikisha Morrison Kamati ya Maadili kwa kusaini mkataba na klabu ya Simba wakati shauri la mgogoro wa mkataba wake na Yanga likiwa bado linasikilizwa
Akizungumza mapema leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, Kichere Mwita Waissaka amesema Kamati yake ilikutana Jumamosi na Jumapili iliyopita lakini hawakujadili shauri la Morrison kwa kuwa Mwenyewe hakufika
"Pamoja na kujadili mashauri mengine, shauri la Morrison hatukuweza kulijadili kwa kuwa mwenyewe hakufika. Morrison alituma Mawakili wawili kumuwakilisha lakini kutokana na unyeti wa shauri lake, tuliona ni vyema akafika yeye mwenyewe kwani kuna maswala yatahitaji ufafanuzi wake mwenyewe," alisema
"Ifahamike shauri letu na Morrison ni la maadili, tumepewa taarifa kuwa Yanga walifungua jalada Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo Duniani (CAS) kuhusu mgogoro wa mkataba hivyo maamuzi kuhusu mkataba yanaweza kutolewa huko, sisi tunazungumzia suala la Maadili"
Wakati Kamati hiyo ikishindwa kumuhoji Morrison baada kukacha kikao hicho, Yanga ilipeleka malalamiko mengine Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji wakihoji uhalali wa mkataba wa Morrison na klabu ya Simba. Bado kamati hiyo haijatoa taarifa baada ya kukutana hapo jana