Uongozi wa Yanga unasubiri kutambulisha kocha mpya anayechukua mikoba ya Zlatko Krmpotic aliyetimuliwa mwishoni mwa wiki na mabingwa hao wa kihistoria
Juzi Mkurugenzi wa uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said alitaja sababu ya kutimuliwa Krmpotic ni baada ya kutoridhishwa na mbinu zake licha ya kikosi chake kuwa kinafanya vizuri
Inaelezwa Yanga tayari imekamilisha mazungumzo na Cedric Kaze ambaye alipaswa kuja kabla ya Krmpotic lakini alikwamishwa na changamoto ya mkewe kuugua
Kaze ndiye haswa anayesubiriwa kwa hamu, hakuna shaka ndiye anayekwenda kuifundisha Yanga licha ya uwepo wa tetesi za makocha wengine kama Geroge Lwandamina, Hans van Pluijm na Mjerumani Erns Middendorp
Ujio wa Kaze, wanayanga watarajie soka la ushindani sana kutoka kwa timu yao
Ni kocha anayefundisha soka la kushambulia, amefanya kazi ya kufundisha katika Academy za FC Barcelona kwa zaidi ya miaka mitano, hivyo ni kocha mwenye falsafa ya ile 'tiki-taka' yenyewe inayopigwa na akina Pep Guardiola kule Uingereza
Lakini pia, huyu mtu alisoma ukocha na kufanya kazi kule Ujerumani. Ana leseni ya ukocha aliyoipata nchini humo, hivyo kwa upande mwingine tutarajie kuona soka la nguvu
Mashabiki hawakufurahishwa na soka lililokuwa likifundishwa na Krmpotic licha ya kuwa alipata ushindi katika mechi nne kati ya tano alizoongoza kwenye ligi
Sasa watarajie kufurahi kwani huyo kocha ajae maisha yake yote kafundisha soka la burudani na bila shaka hicho ndicho kinakwenda kutokea