Taratibu benchi la ufundi la Yanga linaonekana kuanza kupata kikosi chake cha kwanza kulingana na kikosi kilichotumika katika mechi mbili zilizopita
Katika kikosi kilichocheza na Mtibwa Sugar, Krmpotic alimjumuisha Carlinhos nafasi ya Yacouba Sogne aliyeanza kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar
Mserbia huyo anaonekana kupendelea kutumia mfumo wa 4-3-3 akianza na walinzi wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu
Langoni Metacha Mnata amejihakikishia nafasi baada ya kucheza mechi tatu mfululizo
Walinzi Kibwana Shomari, Yassin Mustafa, Lamine Moro na Bakari Nondo Mwamnyeto hawa wamejiimarisha katika nafasi zao
Eneno la kiungo wapo Mukoko Tonombe, Zawadi Mauya na Feisal Salum, hawa wanaonekana kupata alama nyingi dhidi ya wengine
Ingawa kinachoonekana ni kuwa Krmpotic anawatumia viungo wote watatu katika mechi zilizopigwa nje ya jiji la Dar es salaam
Michael Sarpong ndiye mshambuliaji kiongozi wakati Tuisila Kisinda ameonekana kujihakikishia nafasi ya winga wa kushoto
Katika mechi zilizopita, Krmpotc alimtumia Carlinhos kama winga upande wa kulia ingawa mchezaji huyo asili yake ni kiungo msaidizi wa mshambuliaji 'namba 10'
Krmpotic amelazimika kumtumia Carlinhos eneo la winga ili kunufaika na mipira yake ya krosi ambayo ina madhara makubwa
Hata hivyo ni wazi Krmpotic anaweza kufanya mabadiliko ya kikosi chake kwenye baadhi ya nafasi hasa kwa michezo inayopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Haruna Niyonzima anaonekana kuwa na nafasi ya kuingia kwenye kikosi kama ilivyo kwa winga Farid Mussa ambaye hata hivyo hajaonekana uwanjani kwa siku kadhaa baada ya kuugua
Baada ya kikosi cha kwanza kupatikana, matarajio ya wengi ni suala la muda tu maelewano yatapatikana katika timu na vijana wataanza kucheza soka linaloeleweka zaidi