Inaelezwa kocha mkuu wa Yanga Zlatko Krmpotic bado hajafanya uteuzi wa nahodha wa kikosi chake ambao kwa sasa wachezaji Deus Kaseke, Haruna Niyonzima na Lamine Moro wamekuwa wakibadilishana majukumu hayo
Kabla ya ujio wa Zlatko, Kaseke ndiye aliyekuwa amepewa majukumu yaliyoachwa na Papy Tshishimbi huku Niyonzima akiwa msaidizi wake
Ni utamaduni wa kila kocha anapowasili kwenye timu anaweza kufanya uteuzi wake kadiri anavyoona inafaa
Cheo cha nahodha ni kikubwa katika timu. Huyu ni kiongozi wa wachezaji wenzake na ndiye kiunganishi kati ya wachezaji na uongozi
Lakini pia, nahodha ndiye mwenye jukumu la kuiongoza timu inapokuwa inacheza uwanjani. Ana ruhusa ya kufanya mawasiliano moja kwa moja na waamuzi pale kunapotokea sintofahamu uwanjani
Niyonzima ndiye anayepigiwa chapuo zaidi kukabidhiwa majukumu hayo. Niyonzima ni mmoja wa wachezaji waandamizi kwenye kikosi cha Yanga
Uwezo wake wa kuzungumza lugha tatu, Kiingereza, Kiswahili na Kifaransa inampa nafasi kubwa zaidi kwani yeye anaweza kufanya mawasiliano na wachezaji wote wa Yanga