Winga wa Yanga Tuisila Kisinda amesema bado hajacheza katika kiwango chake cha juu wakati huu akiendelea kuwasoma mabeki wa timu pinzani
Kisinda aliyetua Yanga akitokea klabu ya AS Vita, ni mmoja wa wachezaji wa kutegemewa kwenye kikosi cha mabingwa hao wa kihistoria
Mchango wake umeonekana katika michezo mitatu ambayo Yanga imecheza mpaka sasa kwenye ligi
"Mashabiki wasubiri mambo mazuri kwani bado sijacheza katika kiwango changu. Kuna mambo najifunza hapa Tanzania pamoja na kuwasoma mabeki wa timu pinzani. Mashabiki wasubiri, watafurahi," Kisinda alinukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
Aidha Mcongomani huyo alieleza kutofurahishwa na tabia ya wachezaji kujiangusha uwanjani ili kupoteza muda akirejea mchezo wa ligi kuu kati ya Yanga dhidi ya Mbeya City ambao ulipigwa uwanja wa Mkapa na Yanga kuondoka na ushindi wa bao 1-0
Kisinda amesema hapendezwi na tabia ya aina hiyo kwani anaamini kama mchezaji unapaswa kupambana ili kuisaidia timu yako
"Sipendi kuona wachezaji wanajiangusha ili kupoteza muda. Naamini kila timu inapaswa kujituma uwanjani, kazi ya mchezaji ni kuisaidia timu yake ili iweze kupata matokeo. Sasa inapotokea wachezaji wa timu moja wanajituma lakini wengine wanajiangusha kupoteza muda sio jambo zuri," aliongeza Kisinda