Yanga inaendelea na maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar ambao utapigwa Jumapili ijayo kwenye uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro
Huu utakuwa mchezo wa nne msimu huu kwa mabingwa hao wa kihistoria
Mkufunzi wa Yanga Zlatko Krmpotic amesema wanaendelea kuimarika taratibu na kuwa wataifuata Mtibwa Sugar wakiwa na malengo yaleyale ya kuondoka na alama zote tatu
"Tumeanza na ushindi mchezo wetu wa kwanza ugenini. Nafurahishwa na upambanaji wa wachezaji wangu, muhimu tunahitaji kupata matokeo katika kila mchezo," alisema
Aidha, Mserbia huyo amewataka mashabiki kuwa watulivu kwani anaamini baada ya muda watafurahi
"Bado sijaridhishwa na mambo kadhaa lakini tunapaswa kuhakikisha tunashinda mechi zetu. Kuna kazi tunaendelea kuifanya, ikikamilika wapinzani wetu wajiandae kisaikolojia"
Yanga inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi ikiwa imejikusanyia alama saba baada ya kushuka dimbani mara tatu
Iko nyuma kwa alama mbili dhidi ya vinara wa ligi hiyo KMC ambao jana walipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mwadui Fc
KMC na Azam Fc zimeshinda mechi zao zote tatu walizocheza mpaka sasa msimu huu