Msimu uliopita Kagera Sugar ilikuwa miongoni mwa timu zilizoisumbua Yanga kwenye ligi hata michuano ya kombe la FA
Kocha wa Kagera Sugar Meckie Mexime ni kama alikuwa amezifahamu mbinu za Mbelgiji Luc Eymael hivyo aliweza kumbana vilivyo katika mechi zote walizokutana pamoja na kuwa katika mechi tatu, Yanga ilishinda mbili na Kagera Sugar moja
Kesho Jumamosi Mexime anakutana na Yanga yenye sura mpya ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya kocha mkuu Zlatko Krmpotic
Ni mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkali kila timu ikihitaji matokeo ya ushindi
Kagera Sugar ilipoteza mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania hapohapo uwanja wa Kaitaba wakati Yanga ikishinda bao 1-0 dhidi ya Mbeya City
Msimu huu Yanga imejiwekea malengo ya kushinda ubingwa hivyo kwao, wanahitaji matokeo ya ushindi katika kila mchezo bila ya kujali wanacheza nyumbani au ugenini
Kuelekea mchezo huo, kocha msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi, amesema wamepata nafasi ya kuwasoma wapinzani wao kupitia mechi zao walizocheza msimu huu, hivyo wako tayari kukabiliana nao
Leo Yanga wanafanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa Kaitaba tayari kwa mchezo huo