Ukimuangalia mwili wake unaweza kusema haka katoto kanaingia kufanya nini uwanjani, si watakaumiza!
Lakini Carlos Fernandez 'Carlinhos' anakuwa mtu tofauti kabisa anapokuwa uwanjani
Ni mchezaji aliyebarikiwa kipaji cha hali ya juu. Mpira unapokuwa mguu kwake unaonekana kuwa kitu rahisi sana
Mwili wake usikudanganye, Carlinhos ana msuli wa kupiga mashuti makali. Tayari amedhihirisha hilo katika michezo dhidi ya Aigle Noir na Mbeya City
Carlinhos unaweza kumfananisha na yule kiungo mahiri wa Manchester City Kelvin De Bruyne 'KDB' ambaye msimu uliopita alishinda tuzo ya mchezaji bora wa EPL
Mapema tu, Carlinhos amedhihirisha ni mchezaji hatari sana kwenye mipira iliyokufa
Mpira ya adhabu na kona hapa nchini huchukuliwa kawaida kwa kuwa haionekani kuwa na madhara makubwa
Lakini ujio wa Carlinhos umeiongezea faida Yanga kwenye mipira hiyo, kwani sasa itakuwa mipira muhimu sana kutengeneza nafasi ya kufunga mabao
Carlinhos ameleta kitu tofauti kabisa kwenye ligi ya Tanzania, wapinzani wa Yanga wajiandae tu huyu dogo ni mtu 'mbadi'
Na sasa ndio kwanza ameanza kurejea kwenye makali yake baada ya kukaa nje kwa muda mrefu tangu ligi ya Angola ilipofutwa kutokana na ugonjwa wa corona