Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limewatoza faini ya shilingi milioni tano kila mmoja Msemaji wa Simba, Haji Manara na Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli na Mjumbe wa Kamati ya Sheria ya shirikisho hilo, Zakaria Hanspope kutokana na makosa mbalimbali ya kimaadili huku wakitakiwa kutotenda kosa lolote la kimaadili ndani ya miaka miwili.
Mashauri yaliyokuwa yakiwakabili wadau hao wa soka ni kama ifuatavyo;
HAJI MANARA: Amekutwa na hatia kwa kuingilia majukumu ya Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji wakati wa kesi ya mchezaji Bernard Morrison kwa maneno aliyoyatoa kupitia Wasafi Media.
HASSAN BUMBULI: Amekutwa na hatia ya kusema uongo kwa Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za wachezaji kwamba hawajapeleka nakala ya hukumu ya kamati wakati nakala ilifikishwa kwenye klabu yake siku moja kabla ya yeye kuongea na Wasafi Media.
ZAKARIA HANSPOPE: Amekutwa na hatia katika makosa mawili
(1) Kutoa taarifa ya muenendo wa shauri ambalo lilikuwa linajadiliwa huku yeye akiwa ni mjumbe wa kamati hiyo.
(2) Kuchochea umma kuhusu sakata la mchezaji Bernard Morrison.
Aidha, kamati hiyo imesema wahusika wanaweza kukata rufaa kama hawakuridhishwa na hukumu hiyo