Kiungo mpya wa Yanga Carlos Fernandez 'Carlinhos' anakabiliwa na changamoto ya kutozifahamu lugha zinazotumika hapa nchini ambazo ni Kiswahili na Kiingereza kidogo
Inaelezwa Carlinhos anakabiliwa na wakati mgumu kuwasiliana na wachezaji wenzake kwa kuwa yeye anafahamu lugha ya Kireno tu huku akijaribu kiingereza 'kwa mbaali'
Uongozi wa Yanga umelazimika kumtafutia mkalimani aweze kumsaidia atimize majukumu yake ndani ya kikosi cha Yanga
Mara nyingi ameonekana akiongozana na winga Farid Mussa ambaye aliishia Hispania kwa misimu minne, anaifahamu lugha ya Kihispaniola ambayo haitofautiani sana na Kireno
Nyakati nyingine pia, kocha wa timu ya vijana Said Maulid 'SMG' alipewa jukumu la kumpa mafunzo nyota huyo. SMG alicheza kule Angola kwa zaidi ya misimu mitatu
Mchambuzi mahiri wa soka nchini Edo Kumwembe ameshauri kuwa mchezaji huyo anapaswa asaidiwe ili aweze kufanikisha lengo lililomleta hapa nchini
Lugha ni changamoto ambayo inaweza kumuondoa katika kutimiza malengo yake kama watu wanaomzunguuka hawatamsaidia aweze kuzoea mazingira haraka
"Atafutiwe kijana mjanja wa Kibongo anayejua kuzungumza kireno, aliyewahi kuzamia Brazil au Msumbiji. Awe mshkaji wake wa karibu nje ya uwanja, amtembeze sehemu za starehe na kwingineko"
"Ale chakula anachotaka sio lazima kiwe cha timu, itamsaidia kusettle haraka. Lakini naona watu wanasubiri ashindwe, .ni mchezaji wa kwanza kutoka Taifa lake kucheza hapa, anahitaji msaada ili acheze"
"Ukifurahia yeye kuondoka kwa kushindwa usilaumu wachezaji wetu waliowahi kwenda nje kisha wakashindwa wakarudi. Wengine walikumbana na hali kama hiyo," aliandika Kumwembe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii