Wapo mashabiki wamediriki kuhoji kwa nini mshambuliaji Ditram Nchimbi 'Duma' amejihakikishia nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga licha ya usajili wa nyota wapya wenye uwezo mkubwa
Nchimbi tayari amecheza mechi mbili katika kikosi kipya cha mabingwa hao wa kihistoria
Alianza na mchezo wa kilele cha wiki ya Mwananchi dhidi ya Aigle Noir, ndiye aliyetengeneza bao la pili la Yanga lililofungwa na Michael Sarpong
Lakini pia Nchimbi akapewa nafasi kwenye mchezo wa kwanza wa ligi kuu msimu huu dhidi ya Tanzania Prisons
Ukiangalia kwa umakini, utabaini Nchimbi amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi cha Yanga tangu msimu uliopita
Mjadala ambao nadhani unaweza kuwepo ni ipi nafasi yake sahihi ambayo anapaswa kuchezeshwa, mshambuliaji au winga?
Kwa nafasi ya ushambuliaji hajaonyesha kuwa na madhara makubwa zaidi ya ile kazi ya kuwapa wakati mgumu mabeki, Nchimbi sio mchezaji unayeweza kumkaba kirahisi
Anapotokea pembeni ndiko faida yake huonekana kwani ni mzuri sana katika kutengeneza nafasi za mabao. Krosi zake mara nyingi ni zenye madhara
Sarpong tayari amenufaika na krosi za Duma, akifunga bao maridhawa kwa kichwa kwenye mchezo dhidi ya Aigle Noir
Msimu uliopita David Molinga nae alifunga takribani mabao matatu kutokana na krosi za Nchimbi
Kuna wakati Luc Eymael aliyekuwa kocha wa Yanga aliamua kumtumia kama winga, na wengi walifurahia kazi aliyokuwa akiifanya katika nafasi hiyo
Pengine hata kocha Zlatko Krmpotic angemtumia Nchimbi nafasi ya winga hasa upande wa kulia angeweza kuwa na madhara zaidi kuliko akianza mshambuliaji pacha na Sarpong
Katika mchezo dhidi ya Prisons, alipoingia Yacouba Sogne, Nchimbi alihamishishiwa upande wa kulia na nusura afunge bao kupitia moja ya nafasi alizopata
Nchimbi anapokuwa uwanjani kuna faida timu inapata, kwanza ni mchezaji anayejituma, anasaidia sana katika ukabaji pale timu inapokuwa haina mpira
Lakini pia jina la 'Duma' hakubatizwa kwa bahati mbaya, Nchimbi ni mchezaji mwenye kasi sana
Kama ilivyo kwa Tuisila Kisinda, hawa ni wachezaji hatari sana kwa zile pasi za kupenyezwa, hakuna mabeki wanaoweza kuwadhibiti linapokuja suala la mipira ya kufukuzana