Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said amethibitisha kuwa Yanga inawafuatilia nyota wawili wa Aigle Noir Ndikumana Athumani na Koffi Kouasai
Wachezaji hao walionyesha uwezo mkubwa kwenye mchezo wa kilele cha wiki ya Mwananchi, mchezo ambao Yanga ilishinda kwa mabao 2-0
Awali kulikuwa na tetesi kuwa wachezaji hao wangesajiliwa dakika za majeruhi kabla ya dirisha la usajili kufungwa juzi, lakini Injinia Hersi amesema wasingeweza kuwasajili kwa kuwaona siku moja tu
"Ni kweli hao wachezaji tuliwaona na kuvutiwa nao lakini hatuwezi kukurupuka kuwasajili, mchezaji kumwona mechi moja tu haitoshi, tunawafuatilia na endapo benchi litawahitaji kwa kipindi hicho basi tutawasajili," alisema Hersi
Yanga ina nafasi mbili za kuongeza nyota wa kigeni kwenye usajili wa dirisha dogo mwezi Disemba
Jana Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla alisema wanakusudia kutumia dirisha hilo kuongeza mlinzi wa kati na mshambuliaji