Mshambuliaji mpya wa Yanga Yacouba Songne amesema amejisikia faraja kwa mapokezi aliyopewa na mashabiki wa timu hiyo na sasa yuko tayari kwa mapambano
Songne alitua nchini jana akitokea Burkina Faso, alikutana na nyomi la mashabiki wa Yanga uwanja wa Ndege ambao walimsindikiza mpaka Makao Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Twiga na Jangwani
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Asante Kotoko ya Ghana, amewashukuru GSM pamoja na viongozi wa Yanga kwa kufanikisha ujio wake nchini
"Nimejisikia faraja kuja Tanzania kuichezea Yanga msimu huu. Nawashukuru wote waliofanikisha ujio wangu, viongozi wa Yanga, wadhamini pamoja na mashabiki. Naamini kwa pamoja tutaweza kufanikisha malengo yetu," alisema Songne
Songne hupendelea kucheza namba 10. Pamoja na uwezo wake mkubwa wa kufunga mabao, ni fundi wa kuwatengenezea wengine nafasi
Lakini pia mwamba huyu ni fundi wa kupiga mipira iliyokufa
Amewasili katika wakati mwafaka kwani moja kwa moja ameanza kazi sambamba na kocha mkuu Zlatko Krmpotic ambaye alitua nchini Jumamosi iliyopita