Leo ni siku muhimu kwa mashabiki wa Yanga ambapo pale uwanja wa Mkapa kutakuwa na tukio maalum la kukaribisha msimu. Ni kilele cha shamrashamra za wiki ya Mwananchi iliyoanza mkoani Dodoma wiki iliyopita
Burudani zitaanza mapema tu, wakali wa muziki wa kizazi kipya wakiongozwa na Harmonize watauwasha moto
Baadae kutakuwa na utambulisho wa kikosi cha Yanga kwa ajili ya msimu wa 2020-21 na kisha kufuatiwa na mchezo wa kukata na shoka kati ya mabingwa hao wa kihistoria dhidi ya Aigle Noir kutoka kule Burundi
Huu utakuwa mchezo wa kwanza kwa mashabiki wa Yanga kuishuhudia timu yao mpya 'mbashara', mchezo huu utawapa taswira ya matarajio yao kuelekea msimu ujao
Hili ni tukio la kihistoria, wananchi wamefunga safari kutoka kila pembe ya nchi kuja kulishuhudia
Kwa wachezaji hasa wale wageni, leo ndio watafahamu ukubwa na thamani ya klabu ya Yanga
Ni siku ambayo wachezaji watafahamu wanacheza katika timu ya aina gani na hivyo wajue wana deni kubwa kiasi gani
Hakuna shaka, mashabiki watajitokeza kwa wingi pale uwanja wa Mkapa, mauzo ya tiketi za Royal na VIP yalimalizika tangu jana
Hii inaonyesha wananchi wako tayari kwenda kujumuika pamoja, kuburudika, na kukaribisha msimu mpya ambao kila mmoja anatarajia uwe wa mafanikio makubwa