Msimu uliopita ulikuwa na machungu mengi kwa mshabiki wa Yanga kilio kikubwa kikielekezwa kwenye safu ya ushambuliaji ambayo haikutimiza wajibu wake vyema
Lakini msimu huu dalili njema zinaonekana mapema, mambo yanaweza kuwa tofauti kwani nyota wapya, wameingia wakiwa na mzuka kwelikweli
Wakati Yacouba Sogne akisubiriwa kutua keshokutwa Jumatatu, washambuliaji Michael Sarpong na Waziri Junior wameonekana kuwa tayari kuibeba Yanga huku wakichagizwa na viungo na washambuliaji wa pembeni Fahdi, Deus Kaseke, Tuisila Kisinda na Farid Mussa
Kuna mafundi pale kati wakiongozwa na Abdulaziz Makame, Zawadi Mauya, Mukoko Tonombe, Feisal Salum, Haruna Niyonzima na Carlinhos ambaye ameanza kuonyesha cheche zake mapema tu mazoezini
Safu ya ulinzi safari hii hakuna presha kwani kuna beki bora wa nchi hii kwa sasa Bakari Nondo Mwamnyeto, Lamine Moro, Said Juma na Abdallah Shaibu, lakini kule pembeni walinzi wenye kasi Paulo Godfrey, Kibwana Shomari, Adeyum Saleh na Yassin Mustafa
Kule langoni ndio hatari tupu, Metacha Mnata, Farouk Shikhalo na Ramadhani Kabwili wote wako sawa, wanachuana vikali kuwania nafasi ya kuanza, sasa wakiwa chini ya mkufunzi mahiri wa makipa Vladmir Niyonkuru raia wa Burundi
Miamba hawa kesho Jumapili watakuwa na nafasi ya kuwaonyesha mashabiki wao utayari wao katika mapambano ya kuwania ubingwa wa ligi kuu uliopotea kwa misimu mitatu mfululizo kwa watani zao Simba
Kwa hakika, kama timu, Yanga imeimarika kwani ina wachezaji bora kwenye kila nafasi. Ni timu ambayo inaweza kutoa vikosi viwili vyenye ushindani sawa