Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Dk Mshindo Msolla amesisitiza kuwa bado wanamtambua winga Bernard Morrison kuwa ni mchezaji wao halali tangu Julai 14 baada ya mkataba wake wa miezi sita kumalizika
Akizungumza mkoani Dodoma leo, Dk Msolla amesema klabu ya Simba inapaswa kuwasiliana na Yanga ili wamnunue mchezaji huyo kama wanataka huduma yake
Aidha Dk Msolla amesema keshokutwa Jumatatu, wanapeleka rasmi malalamiko yao kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ili waweze kupatiwa haki yao
"Morrison bado tunamtambua ni mchezaji wa timu yetu kutokana na kusaini naye mkataba Julai 14 kufuatia ule wa awali wa miezi sita tuliomsainisha Machi 20 kumalizika, bado ni mali yetu, hao Simba tunawaomba waje mezani wamnunue"
"Tuna madai yetu ya msingi na ambayo ni haki yetu, keshokutwa Jumatatu ndio tunapeleka mashtaka yetu rasmi kwa fifa ambao wataamua na kutupatia haki yetu ya msingi," alisema Dk Msolla
Yanga ilisajili mkataba wa Morrison kwenye mfumo wa FIFA hivyo hakuna namna klabu ya Simba itamwandikisha mchezaji huyo bila ya sakata lake kuamuliwa na FIFA
Aidha, Yanga iitakapopeleka Malalamiko yake FIFA, TFF watalazimika kupeleka ushahidi wa mapungufu waliyoona katika mkataba huo na wakati huohuo wakiwa ni wao wenyewe walioidhinisha usajili wake Yanga awali na hivyo kusajiliwa kwenye mfumo wa FIFA