Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefungua milango kwa klabu ya Yanga kuomba mapitio (review) ya hukumu dhidi ya aliyekuwa mchezaji wao Bernard Morrison
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Elias Mwanjala amesema kabla ya kwenda Mamlaka za juu, Yanga wanaweza kukata rufaa kwa kamati hiyo na kuomba hukumu hiyo ipitiwe upya
"Kabla ya kwenda CAS kama walivyotangaza, wanaweza kuomba review ya hukumu iliyotolewa na Kamati inaweza kuketi kuipitia tena," alisema Mwanjala katika mahojiano na Wasafi FM
Baada ya Kamati hiyo kutoa hukumu kuwa Morrison ni mchezaji huru baada ya kubaini mapungufu kwenye mkataba wake wa miaka miwili aliosaini na Yanga, mabingwa hao wa kihistoria walieleza kutoridhishwa na hukumu hiyo na kuweka wazi kusudio lao la kwenda Mahakama ya Kimataifa ya usuluhisho wa Michezo (CAS)
Tayari uongozi wa Yanga umeomba upatiwe nakala ya hukumu ili waweze kwenda Mamlaka za juu kuitafuta haki