Kitendo cha klabu ya Simba kumtambulisha winga Bernard Morrison wakati ikielezwa kuwa ana mkataba na Yanga kimewaumiza sana mashabiki
Baya zaidi kitendo hicho kimefanywa wakati shauri la mchezaji huyo kuhusu madai yake ya kutosaini mkataba Yanga yakiwa bado halijatolewa maamuzi na TFF
Hatua hiyo inatoa taswira mbaya, wengi wanajiuliza Simba wametoa wapi ujasiri wa kumtambulisha Morrison wakati wakifahamu bado maamuzi ya kesi yake hayajatolewa na TFF?
Je TFF wamewataarifu kuhusu maamuzi wanayotarajia kuyatangaza na hivyo Simba kutokuona umuhimu wa kusubiri maamuzi hayo?
Ikumbukwe pia Yanga ilipeleka shauri TFF ikiituhumu klabu ya Simba kumrubuni Morrison asaini kunako klabu hiyo. Shauri hilo linaihusu Simba moja kwa moja nalo linasubiri kutolewa maamuzi na TFF
Ushahidi wa shauri hilo upo wazi, Morrison mwenyewe alithibitisha kuwa alipewa dola 5,000 na aliyemtaja kuwa Wakala wa Simba akimshawishi asaini mkataba
Ushahidi mwingine ni kitendo cha Simba kumtangaza Morrison hapo jana, kwani kinathibitisha madai waliyotoa Yanga
Kwa jinsi hili sakata lilivyo, Wanayanga tutafanya makosa makubwa kuwalaumu viongozi wetu kwani ukweli bado haujulikani
Kwa nini mashabiki tuwaamini sana hao Simba ambao hatujui ajenda yao kuliko viongozi wetu?
Mimi binafsi naunga mkono kauli ya uongozi, tusubiri uamuzi wa TFF
Pamoja na kwamba dalili zinaonyesha uamuzi utakuwa upande wa mchezaji, bado Yanga ina nafasi ya kukata rufaa Mamlaka za juu ya TFF, kule FIFA na hata Mahakama ya Usuluhisi wa Masuala ya Michezo (CAS)
Huko ndiko haki sahihi inaweza kupatikana kwani maamuzi yatakayotolewa huko hayataibeba timu yoyote
Ninaamini kuna jambo kubwa lipo nyuma ya cinema hii ya Morrison
Siamini kama GSM au uongozi wa Yanga wanaweza kufoji saini yake, kwa maslahi yapi?
Hawa GSM wametoa zaidi ya Bil 2 kufadhili mchakato wa mabadiliko Yanga, wangeamua fedha hizi wakatumia kusajili Ma Morrison 20 hivi, hivyo hawana sababu ya kughushi saini yake
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Simon Patrick aliwataka mashabiki kuwa watulivu wasubiri hukumu ya TFF, kama haitakuwa upande wao, watakwenda kuitafuta haki Mamlaka za juu zaidi
Alisisitiza kuwa shauri hili litakuwa mwanzo wa Mabadiliko ya mfumo wa uongozi wa soka nchini kwani HAWATAKUBALI
Katika sura nyingine,Β sakata hili ni kama lina lengo la kuwatoa Wanayanga kwenye 'reli'
Kwani siku mbili hizi hakuna mtu anayezungumzia maandalizi ya michakato mingine kuelekea msimu ujao, kila kona ni Morrison tu
Ikumbukwe ni chini ya siku 30 zimebaki kabla ya msimu mpya wa ligi kuu ya Vodacom kuanza
Tuachane na huyu Morrison kwani alijiondoa Yanga pale alipofanya matendo ya kuidharirisha brand ya Yanga
Huyu hata TFF wakimrudisha Yanga, atakaa benchi mpaka mkataba wake utakapomalizika labda ijitokeze timu imnunue
Sidhani kama kuna Wanayanga atakuwa tayari kumuona akivaa tena uzi wa mabingwa hao wa kihistoria
Tusonge mbele, tuziache Mamlaka zinazohusika zishugulike nae, sisi tuendelee na maboresho ya timu yetu kuelekea msimu mpya