Wakati Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iikitarajiwa kutoa maamuzi August 10 kuhusu mvutano wa mkataba kati ya winga Bernard Morrison na Yanga, inaelezwa Mghana huyo amesaini klabu ya Simba na wanakusudia kumtangaza wakati wowote
Kama Simba watafanya hivyo ni wazi watakuwa wanafahamu hukumu inayokwenda kutolewa na Kamati ya TFF siku hiyo ya Jumatatu
Yanga ilishawahi kutoa malalamiko kuwa hawakubaliani na jinsi TFF walivyokuwa wakilishughulikia suala la Mghana huyo, wakiwatuhumu baadhi ya wajumbe kuwa na ajenda za kumpeleka mchezaji huyo klabu ya Simba
Hata hivyo TFF ilikana tuhuma hizo na kusisitiza kuwa haiwezi kuingilia maamuzi yanayofanywa na kamati zake
Wakati Morrison alipeleka malalamiko TFF akikana kusaini mkataba mpya Yanga, mabingwa hao wa kihistoria nao walipeleka malalamiko TFF wakiituhumu klabu ya Simba kufanya mazungumzo na Mghana huyo wakati akiwa na mkataba na Yanga
Yanga huenda ikalipeleka suala hilo FIFA na hata Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi wa michezo (CAS) kama maamuzi hayatawatendea haki