Kocha wa viungo Riedoh Berdien amesema anafurahia maisha hapa Tanzania akiwapa sifa mashabiki wa Yanga kuwa ni mashabiki bora aliowahi kukutana nao katika majukumu yake kwenye soka
Riedoh aliletwa nchini kwa mapendekezo ya Luc Eymael aliyekuwa kocha wa Yanga ambaye alitimuliwa kazi mwanzoni mwa wiki hii
Hata hivyo kocha huyo mtaalam wa mazoezi ya viungo akiwa amewahi kufanya kazi katika mataifa mbalimbali, amesema yeye hajafukuzwa Yanga, anasubiri ujio wa kocha mpya ili aweze kufahamu hatma yake
"Mimi sijafukuzwa, bado nipo hapa Tanzania, nasubiri uamuzi utakaotolewa baada ya Kocha Mkuu kuwasili. Hata hivyo nafurahia maisha hapa, navutiwa na jinsi mashabiki wa Yanga wanavyoipenda na kuiunga mkono timu yao"
"Nimefanya kazi sehemu nyingi barani Afrika, lakini nafikiri sikuwahi kukutana na mashabiki waungwana kama hawa wa Yanga hapa Tanzania," alisema Riedoh
Uongozi wa Yanga unatarajiwa kumtangaza mrithi wa Luc Eymael katika kipindi cha siku 14. Riedoh ameonyesha kuwa tayari kuendelea kuitumikia Yanga kama uongozi utamuhitaji