Nahodha Msaidizi wa Yanga Juma Abdul ameeleza kushitushwa na kuondolewa ghafla kwa kocha Luc Eymael lakini anaamini uongozi wa Yanga utampata mbadala wake haraka
Eymael alitimuliwa na Yanga juzi baada ya kutoa kauli za kibaguzi dhidi ya mashabiki wa Yanga na Watanzania wote kwa ujumla
Abdul amesema kocha huyo alikuwa tayari ameandaa mipango yake kuelekea msimu ujao hivyo kuondoka kwake kunaweza kuwa na athari
"Athari inaweza kuwepo kwa sababu kwa kipindi tulichokuwa nae kuna kazi alikuwa ameifanya na pia tayari alishaweka mipango kuelekea msimu ujao. Lakini sisi kama wachezaji lazima maisha yaendelee, tunafahamu viongozi wameanza kutafuta kocha mwingine"
"Changamoto iliyopo ni kuwa tutahitaji muda kuweza kujifunza mbinu za kocha mpya atakayekuja, lakini pia tunafahamu timu yetu inaweza kuwa na mabadiliko makubwa, wachezaji wapya watakuja hivyo ni wazi tutahitaji tena muda kuweza kupatikana muunganiko, " alisema Abdul
Aidha Abdul ameushauri uongozi wa Yanga kuhakikisha wanampata kocha mwenye vigezo atakayeweza kutengeneza timu katika kipindi cha muda mfupi wa maandalizi kuelekea msimu mpya
"Ninachoweza kuwaambia viongozi wa Yanga wahakikishe wanampata kocha mwenye vigezo vya Kimataifa lakini pia awe na uwezo wa kuimarisha timu ndani ya muda mfupi uliobaki kabla ya kuanza msimu"
"Lakini pia usajili makini unahitajika ili kuepuka changamoto zilizotukumba msimu uliomalizika"
Wachezaji wa Yanga wamepewa mapumziko ya wiki mbili kabla ya kurejea katikati ya mwezi August kuanza maandalizi ya msimu mpya
Uongozi wa Yanga utatumia muda huo kumalizana na wachezaji wake ambao watakuwemo katika kikosi cha msimu ujao