Yanga imedhamiria kwelikweli kuimarisha kikosi chao kuelekea msimu ujao, mabosi wa Kamati ya usajili Yanga chini ya uhisani wa GSM, wanafanya mambo kwa vitendo
Jambo moja la uhakika ni kuwa Yanga tayari imefanikiwa kuwasajili wachezaji wote waliowahitaji, kinachosubiriwa ni wakati mwafaka kwa majembe hayo kuwekwa hadharani
Jana Kaimu Katibu Mkuu Simon Patrick alidokeza kuwa wataanza mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya baada ya wiki mbili hivyo kuanzia August 01, tutarajie kuwashuhudia nyota wa kigeni wa timu hiyo wakitua nchini kukamilisha masuala ya kiofisi kabla ya kuanza majukumu yao ndani ya mabingwa hao wa kihistoria
Achana na Erick Rutanga, Heritier Makambo na Yacouba Sogne ambao inaelezwa wameshamalizana na mabosi GSM, nyota mwingine anayetajwa kuwa njiani kutua Jangwani ni kiungo mkabaji wa AS Vita Mukoko Tonombe
Awali ziliibuliwa tetesi magazetini kuwa jembe hili likuwa limefanya mazungumzo na Simba, lakini taarifa mpya ni kuwa GSM wamepindua meza wakifanikiwa kumshawishi mwamba huyo kutua Jangwani
Juzi Simon aliwaambia mashabiki wa Yanga wahakikishe hawakaukiwi na bando kwani shughuli ya utambulisho itakapoanza itakuwa bandika bandua
Lakini kubwa zaidi wawe tayari na wiki ya Mwananchi, kwani burudani zaidi itapatikana katika tukio hilo