Ukizungumzia wachezaji ambao wanapaswa kuwania tuzo ya mchezaji bora wa msimu, huwezi kukosa kutaja jana la kiungo wa Kagera Sugar Awesu Awesu
Awesu amekuwa na kiwango cha juu sana msimu huu, ameifanya Kagera Sugar kuwa moja ya timu bora sana katika kutandaza soka la kitabuni
Haishangazi kuona jina lake limekuwa miongoni mwa majina ya wachezaji wazawa wanaohusishwa kuwaniwa na mabingwa wa kihistoria, Yanga
Awesu atakuwa mchezaji huru baada ya mchezo wa mwisho wa ligi kuu na mwenyewe ameweka bayana kuwa hatasita kujiunga na Yanga kama mabosi wa timu hiyo watamtimizia mahitaji yake
Yanga wakiwa tayari na mafundi Haruna Niyonzima na Feisal Salum, kama atapatikana Awesu basi eneo la kiungo cha uchezeshaji litakuwa limeiva kwelikweli
Kocha Luc Eymael anapendelea kandanda la pasi fupifupi, Awesu ni mchezaji anayeingia moja kwa moja kwenye mfumo wake kwani akiwa Kagera Sugar yeye ndiye 'injini' katika safu ya kiungo
Hakuna shaka, huu utakuwa usajili wa maana sana kwa Yanga kama watafanikiwa kuinasa sahihi ya mwamba huyu kutoka visiwani Zanzibar