Msimu wa 2015/16 wakati Luc Eymael akiwa kule Rwanda akiinoa klabu ya Rayon Sports, alikuwa akisaidiwa na makocha wawili, Billy Mussa Kombi na Thiery Hitimana ambaye kwa sasa ni kocha Mkuu wa Namungo Fc
Inaelezwa Eymael amependekeza jina la Hitimana kwa mabosi wa Yanga kuwa kocha wake Msaidizi, zipo taarifa kuwa majadiliano baina ya kocha huyo na Yanga yanaendelea
Hata hivyo baada ya Namungo Fc kufuzu kwa michuano ya kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa msimu ujao (CAF CC), haitakuwa rahisi kwa Yanga kumn'goa Hitimana pale Ruangwa
Ingawa mwenyewe amesema amekuja Tanzania kufanya kazi, hivyo hawezi kuchagua ofisi ili mradi tu maslahi yake yatimizwe
"Nimekuja Tanzania kufanya kazi, naweza kujiunga na timu yoyote ambayo tutakubaliana nayo lakini kwa sasa niko Namungo mpaka msimu utakapomalizika. Uamuzi wa kuondoka au kubaki hapahapa nitaufanya wakati huo," alisema Hitimana
Msimu huu Namungo Fc imejipambanua miongoni mwa timu bora kwani pamoja na kukata tiketi ya kushiriki michuano ya CAF katika msimu wake wa kwanza ligi kuu, timu hiyo inasifika kwa kucheza kandanda safi
Katika michezo miwili ya ligi waliyokutana na Yanga, yote ilimalizika kwa matokeo ya sare
Namungo wako nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 64, alama hizi ni juu ya malengo kwa timu inayocheza msimu wake wa kwanza ligi kuu