Ni suala la muda tu beki kisiki Abdallah Shaibu 'Ninja' atatambulishwa kwa mara ya pili kuwa mchezaji halali wa Yanga kwa miaka mingine miwili
Kabla ya kuondoka baada ya kupata fursa ya kwenda kucheza soka Marekani, Ninja alikuwa akiangaliwa kama mbadala halisi wa mkongwe Nadir haroub 'Cannavaro' aliyetundika daruga mwaka 2018
Ninja alitua Yanga akiwa kijana mdogo tu wa miaka 20 na hata sasa umri wake wa miaka 23 bado unampa nafasi ya kuitumikia Yanga kwa muda mrefu kama ilivyokuwa kwa Cannavaro
Mwamba huyu kutoka visiwani Zanzibar, Wanayanga walimshuhudia akiimarika na kuwa mchezaji mahiri aliyeaminiwa na kocha Mwinyi Zahera wakati huo
Zahera alimtumia Ninja kwa 'shughuli chafu' katika zile mechi korofi. Michezo yote dhidi ya Simba msimu uliopita Ninja alitumika kama kiungo mkabaji na shughuli yake wanaikumbuka wale washambuliaji wawili wakongwe wa klabu ya Simba
Kwa sasa Ninja ameimarika kama mchezaji, fursa aliyoipata kwenda kucheza soka Marekani kwa miezi sita, imemfanya awe na sifa ya mchezaji mkubwa
Muda aliokuwa nje ulimpa fursa ya kujifunza mambo mengi, ikiwemo kanuni sahihi ambazo mchezaji unapaswa kuzifuata ili uweze kufanikiwa
Anarejea wakati Yanga ikiwa na changamoto kwenye safu yake ya ulinzi, mkongwe Kelvin Yondani akiwa ukingoni mwa maisha yake ya kusakata kabumbu
Mghana Lamine Moro ndiye anayetegemewa zaidi, lakini ujio wa Ninja umemfanya hata yeye mwenyewe atabasamu alipomshuhudia mazoezini kwa mara ya kwanza
Sasa anakwenda kutengeneza pacha na Shaibu ambaye alipachikwa jina la 'Ninja' kutokana na aina ya soka lake
Wawili hao watatengeneza ukuta wa chuma ambao mbele utalindwa na kiungo mkabaji mahiri Papy Tshishimbi ama James Kotei anayetajwa kuwa kwenye rada za mabingwa hao wa kihistoria
Iyo shughuli ya msimu ujao nadhani haitakuwa ndogo...!