Klabu ya Yanga imebarikiwa kuwa na wachezaji wenye vipaji, wengine wakiwa na uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja kwa ufasaha
Miongoni mwa wachezaji hao ni pamoja na Deus Kaseke ambaye amewashangaza wengi kwa umahiri wake wa kucheza nafasi ya ulinzi wa kulia
Alianza kutumika kwenye nafasi hiyo katika mchezo dhidi ya Azam Fc, kazi yake uwanjani iliwavutia wengi
Jana tena akapewa nafasi hiyo pamoja na kitambaa cha unahodha katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar
Kwa shabiki ambaye kama jana ndio ilikuwa siku yake ya kwanza kumshuhudia Kaseke akiwa dimbani, angefikiri nafasi aliyokuwa akicheza ndio hucheza kila siku kumbe la hasha!
Ametumika kama kiraka tu kutokana na kukosekana kwa nahodha Msaidizi Juma Abdul ambaye alipata majeraha madogo kwenye mchezo dhidi ya Biashara United
Lakini pia Abdul alikuwa na kadi mbili za njano, kama kocha Luc Eymael angemtumia katika mchezo huo na kupata kadi ya tatu, angekosa mchezo dhidi ya Simba
Tangu ligi iliporejea baada ya mapumziko ya corona, mchezaji bora wa kikosi cha Yanga mpaka sasa anaweza kuwa Kaseke