Kabla ya mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Simba ambao utapigwa Julai 12, kikosi cha Yanga kinakabiliwa na mechi mbili za ligi nje ya jiji la Dar es salaam
Mabingwa hao wa kihistoria wanaelekea mkoani Mara ambako siku ya Jumapili wanakabiliwa na mchezo dhidi ya Biashara United
Baada ya mchezo huo Yanga itaunganisha moja kwa moja mkoani Kagera kuikabili Kagera Sugar Julai 09 katika mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkali
Ni juzi tu Yanga imeiondoa Kagera Sugar hatua ya robo fainali ya michuano ya kombe la FA kwa ushindi wa mabao 2-1
Yanga itatumia mechi hizi kama sehemu ya maandalizi kuelekea mchezo dhidi ya Simba ambao kwa hakika mtoto hatatumwa dukani
Kiungo Haruna Niyonzima amewatoa hofu mashabiki wa Yanga akiwahakikishia mechi zote zinazokuja mbeleni watafurahi
"Tumejiandaa vizuri kuwapa mashabiki wetu heshima na mambo mazuri katika michezo iliyobaki. Shukurani sana kwa wana Yanga mashabiki wetu ambao mnaendelea kutuunga mkono," amesema