Uongozi wa Yanga umefunguka kuwa wanaendelea vyema na mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ambapo mpaka sasa tayari wamefanya vikao vinne na washauri wao La Liga
Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amewatoa hofu mashabiki wa Yanga kuwa kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa
Kutokana na masharti iliyoweka nchi ya Hispania kutokana na changamoto ya ugonjwa wa corona, maafisa wa La Liga na Sevilla waliopaswa kuja nchini wameshindwa kufanya hivyo kutokana uwepo wa masharti makali kwa safari za Kimataifa
Hata hivyo teknolojia imechukua nafasi yake kwa La Liga, Sevilla na Yanga kufanya vikao vyao kupitia mikutano ya 'online'
"Mchakato unakwenda vizuri, hadi sasa tumeshafanya vikao vinne na watu wa La Liga na Sevilla, tumewapa taarifa na sasa tumeingia katika hatua ya kuanza kutujengea uwezo kwa idara zetu," Mwakalebela amenukuliwa na tovuti ya Yanga
"Niwaambie Wanachama, mashabiki na Wapenzi kuwa mchakato unaendelea na waendelee kutuunga mkono ili tufaniishe suala hili muhimu kwa maendeleo ya Klabu yetu"