Mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga wametinga nusu fainali ya michuano ya kombe la Shirikisho (ASFC) baada ya kuilaza Kagera Sugar mabao 2-1 katika mchezo mkali uliopigwa uwanja wa Taifa usiku huu
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali, uliishuhudia Kagera Sugar ikitawala kwa muda mwingi lakini Yanga ilitumia vyema nafasi mbili muhimu walizopata kupata ushindi huo
Awesu Awesu alianza kuifungia Kagera Sugar kwenye dakika ya 20 akimchungulia mlinda lango Metacha Mnata aliyekuwa amebana upande mmoja wa lango
Yanga haikuwa na mashambulizi mengi kwenye kipindi cha kwanza lakini kuingia kwa Mrisho Ngasa aliyechukua nafasi ya Ditram Nchimbi kwenye kipindi cha pili, kuliingezea Yanga kasi ya mashambulizi
Alikuwa ni David Molinga aliyeirudisha Yanga mchezoni kwenye dakika ya 52 baada ya kuunganisha vyema kwa kichwa pasi ya Ngasa aliyeuwahi mpira uliogonga mwamba na kumgomgea Molinga kwa kichwa
Katika kipindi cha pili mwamuzi alikuwa na wakati mgumu kuudhibiti mchezo mara kwa mara wachezaji wa Kagera Sugar wakionekana kutokubaliana na maamuzi yake
Kwenye dakika ya 76 Yanga ilizawadiwa mkwaju wa penati baada Ngasa kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari
Deus Kaseke aliukwamisha mpira wavuni na kuihesabia Yanga bao la pili
Kuingia kwa bao hilo kulipelekea mchezo kuwa mgumu vijana wa Kagera Sugar wakija juu kusaka bao la kusawazisha
Hata hivyo nyota hao walishindwa kujidhibiti na kufanya matukio mengi yasiyo ya kiungwana ambapo Awesu Awesu alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kutumia lugha mbaya kwa mwamuzi
Hakika ulikuwa mchezo mgumu, lakini Yanga imefanikiwa kuvuka hatua hii sasa ikimsubiri mshindi wa mchezo kati ya Simba dhidi ya Azam Fc hapo kesho
Katika mchezo uliopigwa mapema, Namungo iklitinga nusu fainali baada ya kuichapa Alliance Fc mabao 2-0